Juma Thomas ZANGIRA: Mtanzania Wa Kwanza Kushtakiwa Nchini Tanzania Kwa Kosa la UJASUSI
UTANGULIZI
Moja ya changamoto zinazoikabili Tanzania ni ukosefu wa kumbukumbu kuhusu watu/matukio muhimu. Tatizo hilo limechangiwa na ukweli kwamba uandishi, hususan uandishi wa vitabu, bado haujapata mwamko wa kutosha nchini Tanzania.
Ni kwa kutambua changamoto hiyo, mwandishi ameanzisha mfululizo wa vijitabu vitakavyokuwa vikieleza kuhusu watu/matukio mbalimbali, hususan kuhusu Tanzania, lakini pia wakati mwingine kuhusu sehemu nyingine duniani.
Kijitabu hiki cha kurasa chache tu ni cha kwanza kabisa katika mfululizo huu.
Moja kati ya kesi kubwa za kihistoria nchini Tanzania ni ile kesi ya UJASUSI (ESPIONAGE) iliyomhusu Bw. JUMA THOMAS ZANGIRA ambayo ilirindima nchini mwaka 1977. Hii ilikuwa ni kesi ya aina yake iliyowaacha wananchi wakiwa hawaamini maskio yao kwani hii ilikuwa ni kesi ya kwanza ya ujasusi nchini.
Siku ya Jumapili, tarehe 25.9.1977, Radio Tanzania Dar Es Salaam, katika taarifa yake ya habari saa mbili usiku, ilieleza kwamba Bw ZANGIRA atapelekwa mahakamani kesho yake,
jumatatu. Hata hivyo, RTD haikutaja atapelekwa mahakama ipi. Kwavile wananchi walizoea kwamba washtakiwa wa makosa ya jinai hupelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jumatatu asubuhi…